Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Bakari Mhina.
Na Pendo Fundisha, Mbeya
WANAUME zaidi ya 300,000 wenye umri kati ya miaka 10 na kuendelea,
wamefanyiwa tohara mkoani Mbeya na Songwe ikiwa ni sehemu ya harakati za
Serikali kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) nchini.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Bakari Mhina, alisema hayo juzi
wakati wa uzinduzi wa kondomu ya kiume ya Zana inayotolewa na Serikali.
Alisema idadi hiyo ni sawa na asilimia 80 huku lengo la Serikali ni
kufanya tohara kwa wanaume wapatao 400,010 hadi kufikia mwakani ili
kufikia asilimia 100.
“Tafiti zimebainisha kwamba asilimia kubwa ya wanaume ambao
hawakufanyiwa tohara wapo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya
magonjwa ya ngono ukiwamo Ukimwi na ndiyo sababu Serikali iliazimia
kuendesha zoezi hili la tohara bila gharama yoyote.
“Kwa mujibu wa takwimu za utafiti uliofanyika nchini kabla ya Mkoa wa
Mbeya kugawanywa, mkoa huo ulishika nafasi ya tatu kwa kuwa na
maambukizi makubwa na ulikuwa na asilimia tisa, huku ukiwa umetanguliwa
na mikoa ya Njombe wenye asilimia 14 na Iringa asilimia 9.1,” alisema.
Akizindua kondomu hiyo kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya,
William Ntinika, alisema licha ya kondomu kupunguza maambukizi ya
Ukimwi, pia zinasaidia kuepuka mimba zisizotarajiwa na aliwataka
wahusika kuhakikisha wanazisambaza kwa walengwa.
“Kondomu hii ya Zana imezinduliwa Mbeya kutokana na kuonekana kuwa ni
miongoni mwa mikoa inayoongoza kuwa na kiwango kikubwa cha watu
walioambukizwa virusi vya ugonjwa wa Ukimwi,” alisema.
Awali akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mratibu wa Afya Kitengo cha
Ukimwi Mkoa wa Mbeya, Dk. Francis Phily, alisema hadi sasa mkoa
umesambaza kondomu ya Zana milioni 1.5 katika wilaya mbili.
CHANZO GAZETI LA MTANZANIA
No comments:
Post a Comment