MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amesema, wanafunzi wengi wa shule
ya Kutwa Mbeya, wanavuta bangi katika eneo la shule ya msingi Azimio na
huwafanyia fujo walimu.
Akizungumza katika kituo cha redio, Makalla alisema uongozi wa mkoa
umeiagiza bodi ya shule, ichukue hatua ya kurejesha nidhamu katika shule
hiyo kwa kuwa haiwezekani mwanafunzi kuwa juu ya mwalimu.
Alisema adhabu iliyotolewa ni kubwa, lakini lipo tatizo la wazazi
kushabikia mambo kwa kutetea watoto wanapokosea, aliwataka wazazi
wasiwashabikie watoto kwa kuwa wanatengeneza kizazi kisichokuwa na
malezi mazuri.
"We jiulize kwamba je wanafunzi wale walioko pale wananidhamu ya
kutosha na walimu ndio chanzo? Wakati tukio hili linaendelea kuchunguzwa
na Polisi, hali ya nidhamu kwa wanafunzi wa kidato cha tatu na cha nne
wa Mbeya Day (Shule ya Kutwa Mbeya) ni mbaya.
Kwa hiyo serikali lazima ichukue hatua ya kurejesha nidhamu kupitia
bodi ya shule lazima tushirikiane kurejesha nidhamu, kuna watoto pale,
tayari tunayo majina ya watoto wanakwenda kuvuta bangi shule msingi
Azimio, wakifika pale ni kufanya vurugu, kwa hiyo tunachukua hatua ya
kurejesha hiyo nidhamu," alisema Makalla.
Alisema wakati mambo mengine ya miongozo na taratibu za Wizara ya
Elimu yakiendelea, uchunguzi wa vyombo vya dola utaendelea. Alisema
hataki jambo kama hilo litokee tena na kutaka ifike mahali wanafunzi
wengine wasiweze kuwafanyia fujo walimu.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Profesa
Joyce Ndalichako amesema ni muhimu kusimamiwa na walimu na mwanafunzi
mwenyewe kujenga mazingira kwamba haendi shule kwa ajili ya kuadhibiwa
bali kusoma.
Alisema malezi yanaanzia kwa wazazi, hivyo ikiwa wazazi nao
hawatekelezi wajibu hao, huchangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa
maadili na nidhamu kwa watoto.
Alisema pamoja na kwamba adhabu ile haikustahili, lakini lipo tatizo
kubwa kwa wanafunzi kutokuwa na nidhamu kwa walimu, jamii na wenzao.
Alisema mwalimu anapaswa kutambua kuwa ameingia kwenye kundi la
walezi, hivyo kujenga ukaribu na mwanafunzi na kumsaidia kwa kusimamia
ipasavyo nidhamu na si kuweka mbele adhabu. Neno la Ten/Met Shirika la
Ten/Met pamoja na kulaani ukatili aliofanyiwa mwanafunzi huo, pia
lilishauri mifumo ya elimu ya ualimu na malezi ya wanafunzi iimarishwe.
Mratibu wa Ten/Met, Cathleen Sekwao alisema huenda haiba ya uchaguzi
wa aina ya wanafunzi wa kusoma ualimu, haizingatiwi vya kutosha siku
hizi.
"Matokeo ni kwamba watu wasio na haiba ya ualimu hujiunga na kozi ya
ualimu na kufanya yasiyostahili. Huenda pia mtaala wa mafunzo ya ualimu
unakazia zaidi masomo kuliko malezi," alisema Sekwao katika tamko lake
juzi.
Alipendekeza wanafunzi wanaochaguliwa kuingia ualimu, wapendekezwe na
shule wanakomalizia elimu ya sekondari na mtaala wa elimu ya ualimu,
uangaliwe upya hasa kipengele cha malezi ya wanafunzi, maadili na
muongozi wa uhusiano baina ya mwalimu na mwanafunzi.
Aidha, alipendekeza Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kutoa mafunzo ya
mara kwa mara kujenga uhusiano kati ya mwalimu na mwanafunzi.
Awali, akizungumza na gazeti hili, Rais wa CWT, Gratian Mukoba
alisema walimu vijana wa sasa wamekosa kujitambua kuwa wanapokuwa walimu
wanaingia katika kundi la walezi, hivyo wanapaswa kulea zaidi ya
kufikiria kuadhibu.
Mukoba alisema adhabu ni hatua ya mwisho kwa mwanafunzi na kushauri
walimu kujenga ukaribu na wanafunzi katika misingi ya kutaka kujua
tatizo linalomfanya mwanafunzi kuwa na tabia mbaya na sugu.
Aliwataka walimu vijana kuweka kando mihemuko, kutumia miongozo na
sheria katika kufanyakazi zao kwa weledi, badala ya kugeuka mabondia na
vituko kwa jamii hivyo kusababisha wanafunzi kutowaheshimu.
Utoaji wa viboko Wakati hayo yakibainishwa, Serikali imesema Waraka
wa Elimu wa mwaka 2002 unaelekeza utoaji wa adhabu ya viboko kwa
wanafunzi kuwa ni lazima kuidhinishwa na mwalimu mkuu kwa maandishi,
huku kukiwa na daftari linaloonesha idadi ya viboko, alivyopigwa
mwanafunzi na mwalimu aliyemchapa.
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imeweka
bayana utoaji wa adhabu hiyo, lakini wakiwataka wanafunzi kujiepusha
kufanya makosa mbalimbali, yatakayosababisha kupigwa viboko kwani
shuleni wameenda kwa ajili ya kusoma.
Kaimu Kamishna wa Elimu, Nicholaus Buretta alisema hayo juzi
alipozungumzia Waraka huo Namba 24 wa mwaka 2002, ulioanza kutumika
Desemba Mosi mwaka jana, unaoelekeza adhabu zinazopaswa kutolewa kwa
mwanafunzi kwa utovu wa nidhamu uliokithiri au kufanya makosa ya jinai.
Alisema adhabu hiyo ya viboko, hutolewa kwa kuangalia ukubwa wa kosa,
jinsi ya mwanafunzi, afya yake pamoja na kuhakikisha viboko hivyo
havizidi vinne kwa mwanafunzi, tena hutolewa na mwalimu mkuu au mwalimu
aliyethibitishwa na Mwalimu Mkuu kwa maandishi. “Hatuhamasishi adhabu
hii kwa wanafunzi bali wanafunzi wanatakiwa kujua kuwa wamekuja shuleni
kusoma na hawajaja kuchapwa viboko hivyo lazima wajiepushe kufanya
makosa yatakayosababisha kuchapwa.
Tunahamasisha mahusiano bora kati ya mwalimu na mwanafunzi ambayo ni
yale ya kama mzazi,” alisema Buretta. Alisema katika mahusiano hayo
mtoto anatakiwa kuwa rafiki wa mwalimu bila kukiuka taratibu za ulezi
kwa lengo la mwanafunzi asimuone mwalimu wake kama simba ambaye wakati
wote anamuogopa. Buretta alisema serikali hivi sasa ina mikakati ya
uboreshaji elimu inayowekwa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu.
Alisema watahakikisha wanafikia wastani wa darasa moja kuwa na
wanafunzi 1:40 hadi 45 ili kufikia malengo. Adhabu ya viboko mashuleni,
inasimamiwa na sheria ya adhabu kwa wanafunzi mashuleni ya mwaka 1979.
Sheria hiyo ilikuwa inatoa fursa ya mwanafunzi kuadhibiwa viboko
visivyozidi sita. Hata hivyo, mwaka 2000 Serikali ilihaulisha sheria
hiyo na kuweka idadi ya viboko kwa mwanafunzi visizidi vinne na adhabu
hiyo itolewe na mwalimu mkuu.
Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko, Gloria Tesha na Shadrack Sagati
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
No comments:
Post a Comment