TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI “PRESS RELEASE” TAREHE 28.07.2017.
Jeshi
la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria
zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu
na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada
hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa
ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu.
Mafanikio yaliyopatikana kutokana na misako/doria ni kama ifuatavyo:-
KUKAMATWA KWA WAHAMIAJI HARAMU RAIA WA ETHIOPIA.
Mnamo
tarehe 27.07.2017 majira ya saa 16:30 jioni, Jeshi la Polisi Mkoa wa
Mbeya likiwa katika msako/doria huko katika Kijiji na Kata ya Lupa,
Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya lilifanikiwa
kuwakamata watu wawili raia wa Ethiopia wakiwa wameingia nchini bila
kibali.
Wahamiaji
hao haramu walifahamika kwa majina ya 1. TATIOS TOQKSO [30] na 2.
MITEKU ESUMO [20]. Wahamiaji hao walikamatwa wakiwa wanasafirishwa
kwenye Gari yenye namba za usajili T. 810 AQY aina ya Scania Basi
lililokuwa likitokea Tabora kuelekea Mbeya ambalo lilikuwa likiendeshwa
na dereva aitwaye ABDUL SUDENI [43] Mburush na Kondakta aitwaye IBRAHIM
BAKARI [28] wote wakazi wa Tabora.
Watuhumiwa
wote wahamiaji haramu wawili raia wa Ethiopia na wasafirishaji wawili
kwa pamoja wanashikiliwa na Polisi. Upelelezi unaendelea
KUKAMATWA KWA WAHAMIAJI HARAMU RAIA WA ETHIOPIA.
Mnamo
tarehe 28.07.2017 majira ya saa 03:30 usiku wa kuamkia leo, Jeshi la
Polisi likiwa katika Msako/Doria huko Check-Point Igawa iliyopo Tarafa
ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya, lilifanikiwa kuwakamata
Waethiopia watano (5) kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.
Wahamiaji
hao haramu ni walitambulika kwa majina ya 1. BIRAMU DEISSE [25] 2.
TAPAGI JOBORO [23] 3. BIRHUN ASHOZU [35] 4. TILANU MIFKUUN [23] na 5.
ZARYUN JILIMWA [32] wote raia wa Ethiopia.
Wahamiaji
hao haramu walikuwa wanasafirishwa kwa miguu na Mtanzania ambaye
alifahamika kwa jina la RASHID NDIDI [20] Mkazi wa Dodoma ambaye ndiye
alikuwa mwenyeji wao na walikuwa wakisafiri porini. Upelelezi
unaendelea.
KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI.
Mnamo
tarehe 27.07.2017 majira ya saa 16:00 jioni, Jeshi la Polisi kwa
kushirikiana na askari wa TANAPA walifanya msako huko katika Pori la
hifadhi ya Taifa la Ruaha lililopo Kijiji na Kàta ya Nyamlala, Tarafa ya
Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya, walifanikiwa kukamata
Pikipiki 06 ambazo wahusika wake walikimbia na kuzitelekeza.
Kati
ya Pikipiki hizo, mbili zilikuwa hazina plate namba na nyingine
zilikuwa na za usajili MC 386 BHW aina ya Kinglion, MC T.799 CTW aina ya
T-Better, MC 755 ADJ, T.461 BZE. Aidha Pikipiki hizo baada ya
kukaguliwa zilikutwa na Nyara za Serikali ambazo ni Ngozi moja ya Simba
na vipande 15 vya meno ya Tembo. Upelelezi na ufuatiliaji unaendelea ili
kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hili.
WITO:
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi MOHAMMED R. MPINGA
anatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za mtu/watu wanaowatilia mashaka
popote iwe ni kwenye vyombo vya usafiri au hata katika makazi yao, kutoa
taarifa katika vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya ufuatiliaji
na uchunguzi zaidi. Aidha anatoa rai kwa madereva na wamiliki wa vyombo
vya usafiri kuchukua tahadhari pindi wanaposafirisha abiria na kutoa
taarifa mapema kwani wapo baadhi ni wahamiaji haramu.
Imesainiwa na:
[MOHAMMED R. MPINGA – DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA

No comments:
Post a Comment