Social Icons

Friday, July 21, 2017

WAZIRI MKUU AAGIZA BIASHARA ZA MAZAO ZISIMAMIWE VIZURI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kusimamia biashara ya mazao mbalimbali katika maeneo yao ili wakulima waweze kupata tija.

Pia amesema Bodi ya Mazao Mchanganyiko inazunguka nchi nzima kupata taarifa za bei ya mazao hayo ili kujirisha iwapo wanunuzi wa mazao mchanganyiko ya wakulima kama wananunua kwa bei inayostahili.

Alitoa agizo hayo jana (Alhamisi, Julai 20, 2017) wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ilasilo kilichoko katika mpaka wa mkoa wa Mbeya na Songwe alipokuwa njiani kuelekea wilayani Songwe kwa ajili ya ziara ya kikazi.

Alisema kwa sasa bodi hiyo inazunguna nchini kote kutafuta taarifa za bei za mazao ili kubaini bei zinazotumiwa na wanunuzi wa mazao hayo kama zinastahili baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima wa eneo hilo.

“Wakulima msikubali kuuza mazao ovyo, wekeni na akiba ya chakula. Pia  Bodi ya Mazao Mchanganyiko itakuja hapa kwa kuwa sasa inapita sehemu mbalimbali kupata taarifa za bei za mazao pamoja na kuwatafutia masoko yenye tija.”

Pia Waziri Mkuu aliwaagiza watu wote wanaohusika na suala la usambazaji wa pembejeo kuhakikisha wanazifikisha kwa wakulima katika kipindi kisichopungua muda wa miezi miwili kabla ya kuanza kwa msimu ili kuwaondolea changamoto ya uchelewashwaji wa huduma hiyo

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Bi. Chiku Gallawa alitaja changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya kilimo ni kutokuwepo kwa soko la uhakika la mazao pamoja na uingizwaji wa pembejeo zisizofaa katika mkoa.


Alisema tayari mkoa umechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hizo kwa kuhimiza matumizi ya teknolojia ya kisasa kama matumizi ya mbegu bora zinazostahimili hali ya hewa iliyopo na zinazokomaa kwa muda mfupi.

Pia wataalamu wa kilimo walichunguza pembejeo zinazotumika katika mkoa huo ambapo walibaini asilimia 60 ya viuatilifu na asilimia 20 hadi 30 ya mbegu zinazouzwa madukani na kutumiwa na wakulima katika wilaya za Momba na Mbozi ni bandia.

Alisema matokeo ya kutumia pembejeo hizo yalisababisha mavuno ya mahidi kupungua kutoka magunia 25 hadi magunia manane kwenye ekari moja katika msimu wa kilimo wa mwaka 2012/2013.

Mkuu huyo wa Mkoa alitaja mikakati waliyojiwekea katika kukabiliana na changamoto hiyo kuwa ni kufanya ukaguzi kwenye maduka yote yanayouza pembejea pamoja na kutoa elimu ya kutambua pembejeo zisizifaa ili watoe taarifa mapema na wahusika wachukuliwe hatua.

No comments:

Post a Comment