Imeandikwa na Nebart Msokwa (Mbeya) na Paul Mabeja (Dodoma).
WAKATI kuungua kwa soko la Sido jijini Mbeya
kukisababisha kilio kwa mamia ya wafanyabiashara waliopoteza mali na
maeneo yao ya kujiingizia kipato halali, mapya yameibuka kuhusiana na
namna moto huo ulivyosambaa kwa haraka.
Aidha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ameelezea kushtushwa kwake na tukio hilo na kuamuru kufanyika kwa uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo na mwishowe hatua zaidi kuchukuliwa.
Soko hilo lililokuwa na maduka na vibanda vya biashara zaidi ya 3,000, lilishika moto na kuteketea kwa kiasi kikubwa juzi usiku huku baadhi ya waathirika wakibaki na maswali mengi na wengine wakiwa kama hawaamini juu ya kile kilichotokea.
Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya mashuhuda walisema kuwa namna moto huo ulivyoanza, kusambaa kwake na pia historia ya jiji la Mbeya juu ya matukio hayo, ni miongoni mwa mambo yaliyowaacha midomo wazi wasijue ni nini hasa chanzo cha kujirudia kwa maafa ya aina hiyo.
Ilielezwa kuwa moto huo ulianza majira ya saa 2:15 usiku katika moja ya mabanda ya kuuzia nafaka na kusambaa kwingine kote huku jitihada za kuudhibiti ili usisambae zaidi zikiishia kugonga mwamba.
“Kwakweli huu moto ulikuwa na maajabu yake. Taarifa za kutokea kwake zilianza kama masihara, kutahamaki tayari umeshasambaa soko zima licha ya kuwapo kwa jitihada nyingi za kuuzima,” mmoja wa mashuhuda aliiambia Nipashe.
Maafa ya juzi usiku ni ya pili kutokea katika soko la Sido baada ya kuwahi kuungua pia mwaka 2011 na pia ni mara ya nne kwa masoko ya Mbeya kuteketea kwa moto. Matukio mengine aina hiyo yalishatokea katika masoko ya Mwanjelwa (mwaka 2006) na Soko la Uhindini lililoungua mwaka 2010.
“Sasa kuna haja ya kufanyika kwa uchunguzi wa kina ili kujua undani wa matukio haya. Haiwezekani kila mara iwe Mbeya tu…
Tanzania kuna masoko katika miji yote lakini matukio haya hutokea kwetu tu.
Lazima kuna sababu na hiyo inapaswa kujulikana ili kuepuka majanga ya aina hii,” aliongeza mmoja wa wafanyabiashara.
Katibu wa Soko hilo, Lainus Ngogo, alisema maafa yaliyotokea ni makubwa kwao kutokana na ukweli kuwa kati ya maeneo ya biashara 3,136 yaliyopo, yaliyonusurika na moto huo ni 140 tu na kwamba moto huo umeleta hasara kubwa kwa wafanyabiashara.
VIBAKA, MIUNDOMBINU LAWAMANI
Baadhi ya wafanyabiashara waliounguliwa na maduka na kila kitu kilichokuwamo ndani yake, walitaja sababu za kuwapo kwa madhara makubwa ya ajali hiyo kuwa ni vibaka na miundombinu mibovu ya barabara ndani ya soko hilo.
Wakisimulia zaidi, baadhi ya waathirika hao walisema kuwa walishindwa kuokoa mali zao kutokana na miundombinu ya barabara kutowezesha magari ya zimamoto na uokoaji kuingia huku pia vibaka wakiishia kukimbia kusikojulikana na baadhi ya mali walizojaribu kuziokoa.
Mmoja wa waathirika hao, Shukuru Mtewele, alisema wakati wakijaribu kuokoa mali, liliibuka kundi la vibaka lililokuwa likivamia na kupora baadhi ya mali ambazo zilikuwa bado hazijashika moto na kutimua nazo mbio.
Aidha, alisema moshi mkubwa uliokuwa umetanda ulichangia pia kukwaza jitihada za uokoaji na badala yake kukimbia ili kunusuru maisha yao.
“Tulijaribu kuokoa baadhi ya mali lakini baada ya kundi la vibaka kuvamia na kuanza kupora, tulishindwa kukabiliana nao. Pia magari ya zimamoto yalishindwa kuingia kutokana na vibanda kubanana,” alisema Mtewele.
Katibu wa Soko hilo, Ngogo, alikiri kuwa magari ya zimamoto yalikuwa yakiishia kusimama kwa mbali na kwamba, baadhi ya askari wa kikosi hicho hawakuwa wakizingatia ushauri waliokuwa wakipewa juu ya namna ya kufika ndani ya soko kulikokuwa na moto.
Aidha, alilalamikia wahalifu waliojitokeza kufanya uporaji kuwa pia walichangia kuongeza hasara kwa wafanyabiashara.
Meya wa Jiji la Mbeya, Mchungaji David Mwashilindi, ambaye alifika kuwafariji waathirika akiwa ameongozana na Mkuu wa Wilaya hiyo, William Ntinika, alisema kuungua kwa soko hilo ni hasara kubwa kwa wananchi pamoja na Serikali.
Mwashilindi alisema Halmashauri ya jiji hilo ilikuwa inategemea mapato kutoka katika Soko hilo na hivyo kuungua kwake imekuwa pigo kubwa kwani imepunguza vyanzo vya mapato.
Alisema wanawapa pole wananchi na kwamba, wanakusudia kuitisha kikao cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili tukio hilo na namna sahihi ya kuwasaidia wafanyabiashara hao.
Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, Ntinika, alisema anakusudia pia kuitisha Kikao cha Kamati yake ili kuunda tume ya kufanya tathmini ya hasara iliyosababishwa na moto huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga, alisema hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo na kwamba uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini chanzo chake.
Vilevile, alisema hakuna mtu aliyepoteza maisha kwenye tukio hilo ambalo limeacha vilio na simanzi kwa wafanyabiashara.
WAZIRI MWIGULU ANENA
Akizungumzia tukio la moto wa soko la Sido mbele ya waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Mwigulu alielezea masikitiko yake na kuagiza Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya kufanya uchunguzi wa kina ili chanzo cha ajali hiyo kijulikane.
Alisema kuna umuhimu wa kupata majibu ya kina juu ya tukio hilo ili mwishowe kupata suluhu ya matukio mengine ya aina hiyo jijini Mbeya na kwingineko nchini.
“Kipindi cha nyuma palikuwapo na matukio ya moto katika maeneo mbalimbali lakini yalikomeshwa… lakini kama mlivyosikia jana (juzi), Mbeya tena moto umetokea na kuteketeza soko,” alisema Nchemba.
“Niagize kuanzia leo, halmashauri zote nchini pamoja na idara zinazohusika na ujenzi wa makazi kulishirikisha jeshi la zimamoto katika hatua za awali za ujenzi ili kusaidia kuwapo kwa miundombinu mizuri inayoweza kuingilika mara matukio kama hayo yanapotokea,” alisema Mwigulu.
CHANZO; NIPASHE

No comments:
Post a Comment