Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali (pichani) imedhamiria
kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo
mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya ilitengewa Sh
bilioni 2.72 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji.
Alisema mkakati huo unatekelezwa kupitia Kampeni ya Rais John
Magufuli ya kumtua mama ndoo, wananchi katika maeneo yote nchini
watapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400
kutoka kwenye makazi yao. Waziri Mkuu aliyasema hayo juzi alipozungumza
kwa nyakati tofauti na wananchi wa halmashauri za Rungwe na Busokelo
katika mikutano ya hadhara aliyoifanya Kandete na Tandale katika Wilaya
ya Rungwe mkoani Mbeya.
Majaliwa alisema Mkoa wa Mbeya umetengewa Sh bilioni 10.383 kwa ajili
ya utekelezaji miradi mbalimbali ya maji, ambazo kati yake Sh bilioni
2.72 zinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maji kwenye
Wilaya ya Rungwe. Waziri Mkuu alitaja mradi mwingine unaotekelezwa
wilayani Rungwe ni pamoja na mradi wa maji wa Masoko wenye thamani ya Sh
bilioni 5.3, utakaohudumia jumla ya vijiji 15.
“Mradi huu ni miongoni mwa miradi inayojengwa chini ya Programu ya
Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa fedha za ndani,” alieleza. Alisema mradi
huo utakapokamilika utawanufaisha wananchi wapatao 19,624 katika vijiji
vya Bulongwe, Ngaseke, Igembe, Ntandabala, Lupando, Bujesi, Lufumbi,
Nsyasa, Ikama, Itagata, Busisya, Mbaka, Isabula, Lwifa na Nsanga.
Pia Waziri Mkuu alisema wananchi lazima wazingatie Sheria ya
Mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu pamoja na kujenga
kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60 ili kuliepusha
Taifa kugeuka jangwa. Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu aliwaagiza
watendaji kuwachukua hatua watu wote watakaokutwa wakiendesha shughuli
mbalimbali kama za kilimo, ujenzi wa makazi na uchungaji wa mifugo ndani
ya vyanzo vya maji kwa kuwa zinasababisha ukame.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment