Kamanda wa Polisi wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari
POLISI mkoani Mbeya imewafukuza kazi askari wake wawili kutokana na
kuwafanyia vitendo vinavyokwenda kinyume cha maadili wanafunzi wa kike
wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Isuto iliyopo kijiji na
kata ya Isuto, tarafa ya Isangati Wilaya ya Kipolisi Mbalizi mkoani
hapa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Naibu Kamishna wa Polisi,
Dhahiri Kidavashari, askari waliofukuzwa kazi kuwa ni Konstebo Petro
Magana wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Mbeya na Konstebo Lucas
Ng’weina wa Wilaya ya Kipolisi Mbalizi.
Alisema jana kuwa Polisi ilianza ulinzi wa mtihani wa kitaifa wa
kuhitimu kidato cha nne mwaka huu katika shule mbalimbali za Mkoa wa
Mbeya, lakini katika kazi hiyo inayoendelea ya ulinzi wa mtihani kuna
changamoto zilijitokeza.
Alisema Novemba 4, mwaka huu saa 5:30 usiku huko katika shule ya
Isuto, askari hao walituhumiwa kuwafanyia vitendo vibaya kinyume cha
maadili wanafunzi wa kike wa kidato cha nne wa shule hiyo.
“Inadaiwa kuwa, askari hao kwa pamoja wakiwa kwenye ulinzi wa
mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne 2016 waliwatoa kwenye hosteli
wanafunzi wa kike kwa kile walichodai kupiga kelele,” alieleza Kamanda
Kidavashari na kuongeza: “Baada ya kuwatoa wanafunzi hao, waliwapeleka
eneo la kufoleni na kuanza kuwapa adhabu mbalimbali ambazo ni kupiga
push up, kuruka kichura, kushika masikio na kuwachapa viboko sehemu za
makalio vitendo vilivyowasababishia maumivu makali na kusababisha baadhi
ya wanafunzi hao wa kike kuondoka na kurudi majumbani kwao.”
Alisema kutokana na vitendo hivyo, Mkuu wa Shule hiyo, Rose Dihembe
alitoa taarifa kwa uongozi wa Wilaya uliochukua hatua za haraka ikiwa ni
pamoja na kusikiliza malalamiko ya wanafunzi na kuwaondoa askari
waliolalamikiwa ambao baadaye walichukuliwa hatua za kinidhamu.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
No comments:
Post a Comment