Na Eleuteri Mangi-WHUSM, Mbeya
Wadau
wa michezo mkoni Mbeya wametakiwa kuendeleza mshikamano walionao ili
kuifanya sekta ya michezo kuwa chanzo cha kuongeza fursa za ajira kwa
vijana pamoja na wataalamu wengine wa michezo.
Katibu
Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole
Gabriel amesema hayo leo jijini Mbeya alipokuwa akiongea na baadhi ya
viongozi wa vyama vya michezo mkoani humo ikiwa ni moja ya malengo ya
ziara yake ya kikazi mkoani humo.
“Nimefurahishwa
na mkoa wa Mbeya kuwa na mipango ambayo imewafanya vyama vya michezo
kuendeshwa bila kuwa na migogoro, hii ni hatua nzuri imenipa moyo,
mkishikamana vizuri mtafanikiwa sana katika malengo yenu ya michezo”
alisema Prof. Ole Gabriel.
Ili
kuhakikisha michezo inakuwa na tija kwa mkoa wa Mbeya na taifa, Prof
Ole Gbriel ametaka viongozi hao kuwa na mkakati wa kimkoa wa kubadilisha
fikra za watu katika michezo na kutambua kuwa zipo fursa nyingi katika
michezo yote bila kubagua aina ya mchezo.
Awali
akitolea ufafanuzi baadhi ya masuala ya michzo, Prof. Ole Gabriel
ameataka wadau hao kutambua kuwa michezo inaanzia katika ngazi ya chini,
hivyo ni wajibu wao kuendeleza michezo kwa kubadili fikra za wazazi,
vijana, walezi kuipenda michezo kwa kuwa inamchango mkubwa katika ajira,
pato la familia pamoja na uchumi wa taifa.
Akimkaribisha
Katibu Mkuu Prof. Ole Gabriel, Kaimu Afisa Michezo mkoa ambaye pia ni
Afisa Michezo Jiji la Mbeya, Joyce Mwakifwamba amesema kuwa Serikali ya
mkoa inaendelea kushirikiana na wadau wa michezo yote kwa kuzingatia
michezo ni ajira, udugu katika kujenga umoja wa michezo kimkoa na taifa.
Akizunguzia
mpira wa miguu, Katibu Msaidizi Chama cha Mpira wa Miguu Mbeya (MREFA)
Lucas Kubaja amesema kuwa mpira wa miguu unachezwa kuanzia ngazi ya
chini, wilaya zote hadi mkoa.
Kubaja
ameongeza kuwa mkoa unapokuwa na timu nyingi za michezo mbalimbali
katika ligi za michezo hiyo inasaidia kuongeza fursa za kiuchumi kwa
wakazi wa mkoa wa mbeya kunapokuwa na timu zinazokuja kucheza mechi zao
kwenye ligi husika.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti wadau hao wa michezo wamemweleza Katibu Mkuu mwenye
dhamana ya michezo kuwa michezo mingi mkoani Mbeya inakabiliwa na
changamoto ya kutokuwa na viwanja vya michezo hatua ambayo inarudisha
nyuma ukuaji wa michezo mbalimbali.
Vyama
nya michezo vilivyoshiriki mkutano huo huo ni mpira wa miguu (MREFA),
mpira wa pete (CHANETA), mpira wa kikapu, chama cha makocha, riadha,
vishale pamoja na pool table.
Aidha,katika ziara hiyo, Katibu Mkuu pia ametembelea Ofisi
za kanda ya Nyanda za Juu Kusini za Shirika la Utangazaji Tanzania
(TBC) pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa lengo la
kujionea namna wanavyofanya kazi ya kuimarisha mawasiliano katika kanda
hiyo.
No comments:
Post a Comment