Na Eleuteri Mangi-WHUSM, Mbeya
Vijana
wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia, kuboresha na
kuimarisha utamaduni wa namna ya kufikiri kwa mtazamo chanya ili waweze
kujitambua na kutumia fursa walizonazo katika kujiletea maendeleo yao na
taifa kwa ujumla.
Wito
huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makala wakati wa Mahafali
ya pili ya vijana waliohudhuria mafunzo ya ujasiriamali kupitia Programu
ya Mradi wa Uimarishaji wa Maendeleo ya Vijana Vijijini kupitia
Biashara (STRYDE) unaoendeshwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya
TechnoServe.
Katika
mahafali hayo, vijana 907 kutoka Mbeya jiji na Mbeya vijijini
wamehitimu na kunufaika na mafunzo ambayo yamewawezesha kubadili
utamaduni wa namna ya kufikiri hatua ambayo ni mkombozi wa maisha yao
katika kujiletea maendeleo endelevu.
“Ni
vema kuwaza kwa mtazamo chanya badala ya mtazamo hasi, huu ni muda wenu
muafaka wa kubadili maisha yenu baada ya kuhitimu mafunzo haya, ni
lazima kubadilika” alisema Makala.
Mkuu
huyo wa mkoa awasisitiza vijana hao kutumia elimu waliyoipata ya namna
ya kuweka akiba ili waweze kufanya biashara zenye tija katika maisha yao
pamoja na kuwahimiza watumie fursa zilizopo katika maeneo yao kwa
kubadili changamoto zinazokabili jamii wanamoishi kuwa fursa ambazo kwa
ndio njia ya kunyanyua vipato vyao.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Prof. Elisante Ole Gabriel amewapongeza Taasisi ya TechnoServe kwa kuwa
mstari wa mbele kwa kushughulika na vijana ambao ndio nguvu kazi ya
taifa kwa kubadili utamaduni na fikra zao katika kuwekeza kwenye
wajasiriamali wenye tija katika maisha yao.
Prof.
Ole Gabriel ameongeza kuwa Taasisi ya TechnoServe imekuwa mkombozi kwa
vijana wote bila kujali tofauti zao za kijinsia, hali walizonazo
kiuchumi pamoja na vijana wenye mahitaji maalum kwa kuzingatia kila mtu
anauwezo ndani yake akielimishwa ni rasilimali kubwa ya taifa katika
kupambana na umasikini wa fikra na kipato.
Aidha,
Prof. Ole Gabriel amempongeza kijana Irene Mwasile (mwenye ulemavu)
kutoka kikundi cha Umasikini Kwaheri Shilanga, kata ya Ilembo mkoani
Mbeya kwa kuwa miongoni mwa vijana waliofanya vizuri katika mafunzo hayo
kwa kuandika andiko mradi bora na kuwa miongoni mwa kundi la vijana walioshika nafasi ya kwanza na kuzawadiwa mtaji wa shilingi 550,000 pamoja na cheti.
Kwa
upande wake mshindi huyo amesema kuwa anaishukuru Taasisi ya
TechnoServe kwa kumpa mwanga katika maisha yake, hadi sasa ameanzisha
mradi wa kufuga kuku ambao idadi yake hadi sasa ni 30 na matarajio yake
ni kuwa mfugaji wa bora wa kuku nchini na hata barani Afrika.
Katika
mahafali hayo vijana wengine waloshinda katika nafasi tatu za juu
wanatoka katika vikundi 30, vikundi 16 vipo Mbeya jiji na vikundi 14
vipo Mbeya Vijijini, washindi katika vikundi hivyo wamegawanyika katika
makundi matatu ambapo kundi la kwanza washindi wamezawadiwa mtaji wa
shilingi 550,000, washindi wa pili shilingi 350,000 na washindi wa tatu
shilingi 200,000
Hadi
sasa mradi wa STRYDE mkoani Mbeya umewafikia vijana 2193 katika
kuwajengea uwezo kiuchumi tangu kuanzishwa kwake mwaka 2014 ambapo
TechnoServe inatarajia kuwafikia vijana 15,430 ifikapo 2019.
No comments:
Post a Comment