Benny Mwaipaja-WFM, Mbeya
TANZANIA
na Zambia, zimetiliana saini Mikataba Minne kwa ajili ya uanzishwaji
rasmi wa kituo cha pamoja katika mpaka wa Tunduma na Nakonde,
kitakachoanza kufanyakazi rasmi Februari mosi mwaka huu, ili kurahisisha
ufanyaji biashara kati ya nchi hizo mbili
Uamuzi wa kuanzishwa kwa huduma hiyo ijulikanayo kama One Stop Border Post,
ni utekelezaji wa maagizo ya Marais wa nchi hizo Mbili, Waheshimiwa
Dkt. John Pombe Magufuli, na Edger Lungu, waliyoyatoa wakati Rais huyo
wa Jamhuri ya Zambia, Edger Lungu alipofanya ziara ya kikazi hapa nchini
hivi karibuni.
Mikataba
iliyotiwa saini ni makubaliano ya Mwongozo wa Utendaji wa Kituo cha
Pamoja cha Tunduma/Nakonde pamoja na Mfumo wa Urahisishaji Biashara kwa
lengo la kukuza biashara kati ya nchi hizo mbili.
Waliosaini
Mikataba hiyo kwaniaba ya Serikali ya Tanzania, Mjini Vwawa, wilaya ya
Momba, mkoani Songwe, ni Naibu Katibu Mkuu wa Fedha na Mipango, Bi.
Amina Khamis Shaaban na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda, huku Zambia ikiwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Uwekezaji wa nchi hiyo, Bi. Kayula Siame.
Wakizungumza baada ya kutiwa saini kwa mikataba hiyo Makatibu wakuu hao wamesema kuwa Uanzishwaji
wa Kituo cha Pamoja Mpakani Tunduma/Nakonde, utarahisisha ufanyaji wa
biashara kati ya Tanzania na Zambia kwa kupunguza ukaguzi kwani ukaguzi
utafanyika mara moja katika kituo cha kuingia badala ya kufanyika mara
mbili katika nchi zote mbili pamoja na kuongeza makusanyo ya kodi
“Lengo
la kituo hicho pia ni kuifanya biashara kati ya Tanzania na Zambia kuwa
huru lakini ikifuata misingi na taratibu za kufanya biashara mpakani.
Pia kitarahisisha biashara katika eneo la mpakani na kuvutia wananchi na
wafanyabiashara kutoka nchi zote mbili kutumia kituo hiki na kuepuka
kutumia njia zisizo rasmi kupitisha mizigo na hivyo kupunguza ufanyaji
wa biashara za magendo kama si kukomeshwa kabisa” Alisisitiza Bi. Amina
Khamis Shaaban
Alisema kuwa utaratibu huo unatarajia kuona kuongezeka
kwa ushirikiano kati ya taasisi za serikali za nchi hizi kwani shughuli
katika kituo zitakuwa zinafanyika kwa uwazi katika eneo moja.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wa Zambia, Bi. Kayula Siame, amesema kuwa anatarajia kuwa wananchi wa nchi hizo mbili watatumia fursa ya kuwepo kituo hiki kuweza kufanikisha biashara zao na kuepuka kupitisha bidhaa zao kwa njia za magendo ama njia za panya ili kukwepa kukamatwa na vyombo vya dola.
Naye
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Tanzania,
Prof. Adolf Mkenda, alieleza kuwa kuboresha kwa huduma katika Mpaka huo
wa Tunduma na Nakonde utaongeza biashara ya kusafirisha mizigo katoka
Bandari ya Dar es salaam kwenda Zambia na nchi nyingine jirani.
Kwa
upande wake Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw.
Charles Kichere Amesema kuwa huduma hiyo itaanza Februari mosi mwaka
huu kwa kutumia majengo ya forodha yaliyopo katika mpaka huo wa Tunduma
na Nakonde nchini Zambia baada ya kufanyiwa ukarabati na kuwekwa mifumo
ya teknohama, wakati kazi ya ujenzi wa kituo kipya kwa upande wa
Tanzania ukiendelea kujengwa.
Kituo
cha Tunduma/Nakonde kitakuwa kituo cha Tano kufanya kazi baada vituo
vinne kukamilika na kufanya kazi katika mipaka ya Tanzania na nchi
jirani za Kenya, Rwanda na Burundi.
Vituo
hivyo ni Holili-Taveta katika mpaka wa Tanzania na Kenya, Kituo cha
Rusumo katika mpaka wa Tanzania na Rwanda, Mutukula katika mpaka wa
Tanzania na Uganda na Kabanga/Kobela katika mpaka wa Tanzania na
Burundi.
Kwa
upande wa Zambia, hiki kitakuwa kituo cha Pamoja cha Mpakani cha pili
baada ya kituo cha Chilundu kilichopo katika mpaka wa Zambia na
Zimbabwe.

No comments:
Post a Comment