ASASI za kiraia, wabunge na vyombo vya habari vimeombwa kuingilia
kati kukamatwa kwa Watanzania wanane nchini Malawi ambao ni watetezi wa
haki za binadamu.
Watanzania hao kutoka Mtandao wa Kubadilishana Ujuzi na
Kushirikishana taarifa katika masuala ya Kijamii, Kiuchumi na Mazingira
(TUAM) uliopo Songea mkoani Ruvuma, walikamatwa Desemba 20, mwaka jana.
Mratibu wa Kitaifa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC),
Onesmo Olengurumwa alisema Watanzania hao wamekamatwa na wanashitakiwa
kwa mashitaka mawili ya kuingia nchini bila kibali (criminal trespass)
na kupata taarifa bila kibali (carrying out reconnaissance).
Olengurumwa alisema watu hao hawakukusanya taarifa yoyote ambayo
waliikusudia, kwa kuwa hawakufika eneo la tukio na kuelezea kuwa lengo
la ziara hiyo ni kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala ya
mazingira na uchimbaji madini aina ya Urani.
“Watanzania waliokamatwa ni Briton Mgaya, Wakisa Mwansangu, Majidi
Nkota, Christanduzi Ngowi, Ashura Kula, Martin Ndunguru, Wilbert Mahundi
na Rainery Komba ambao awali walishitakiwa kwa makosa ya upelelezi
lakini baadaye yalibadilishwa na kupewa mashitaka ya kuingia bila kibali
na kupata taarifa bila kibali,” alisema Olengurumwa.
Alisisitiza watu hao wamekaa muda mrefu gerezani bila kesi yao
kusikilizwa, hivyo serikali itoe amri ya kutaka watu hao waachiwe huru.
Naye Mwanasheria na Mkurugenzi wa Shirika la Haki za Binadamu na
Biashara (BHRT), Flaviana Charles alisema Watanzania wanakabiliwa na
mashitaka kinyume na Kifungu namba 314 (a) na 2 (3) ya Sheria ya Makosa
ya Jinai ya Malawi pamoja na Kifungu namba 2 (4) cha Sheria ya Madini ya
Malawi.
Charles alisema Watanzania hao, walikuwa wakielekea kijiji cha
Karonga mpakani mwa Tanzania na Malawi kwa mwaliko wa asasi moja
ijulikanayo kama Karonga Business Community ambayo iliratibu ziara hiyo
kwa kushirikiana na Emmanuel Silungwe, mlinzi wa Kampuni ya uchimbaji
urani ya Kayelekera Uranium Mine.
Pia alisema walituhumiwa kwamba Serikali ya Tanzania imewatuma
kuipeleleza Malawi hususan kwenye masuala ya utengenezaji nyuklia, kitu
ambacho si kweli na kwamba mashitaka yao yalibadilishwa zaidi ya mara
nne kutokana na mwendesha mashitaka kutoona kosa la kuwashitaki nalo.
Hata hivyo, alisema kumekuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu kwa
kuwa mwanasheria na Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi, walizuiwa kuwaona
washitakiwa hao na baada ya mazungumzo ya muda mrefu ndio walikubali.
Alieleza kwamba mahojiano kati ya mwanasheria, watuhumiwa na ubalozi
wetu walipoenda gerezani, yalifanyika chini ya ulinzi mkali ambao
uliwafanya washitakiwa hao wasiwe na uhuru wa kujieleza.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
No comments:
Post a Comment