MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi jijini Mbeya imetupilia mbali pingamizi la
upande wa utetezi la kutaka kutosikilizwa kwa ushahidi wa sauti katika
kesi inayomkabili Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi na Katibu wa
Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanual Masonga na kuamuru ushahidi huo
usikilizwe mahakamani hapo.
Mahakamani imefikia uamuzi huo leo baada ya mvutano uliotokea jana
Jumanne ambapo upande wa utetezi ukiongozwa na mawakili Boniface
Mwabukusi na Hekima Mwasipu kuiomba mahakama kutopokea ushahidi huo kwa
madai kuwa una mapungufu ya kisheria.
Baada ya mahakama kukubali utetezi huo mbele ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi, Michael Mteite, shahidi namba tano katika kesi hiyo upande wa
mashtaka Inspekta Joram Magova alitoa ushahidi wa sauti aliyowarekodi
Sugu na Masonga kwa kufunga vipaza sauti ili kusikika kwa ufasaha
mahakamani.
Sugu na mwenzake wanakabiliwa kwa makosa ya kutumia lugha ya fedheha
dhidi ya Rais John Magufuli, mnamo Desemba 30,2017 katika mkutano wa
hadhara walioufanya kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge.
Kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo, askari waliimarisha
ulinzi, huku wakiwazuia wafuasi wa Chadema kuingia katika jengo la
Mahakama kusikiliza kesi hiyo licha ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe na Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Mwakagenda kuingia katika ukumbi
wa Mahakama kufuatilia shauri hilo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho saa 4 asubuhi ambapo upande wa
walalamikiwa utaanza kutoa utetezi baada ya leo upande wa mashtaka
kukamilisha ushahidi wake.
CHANZO GLOBAL PUBLISHERS
No comments:
Post a Comment