ENEO lililokuwa limetengwa ili ijengwe Ikulu ndogo ya Mkoa wa Mbeya
limemegwa na kuuzwa. Limeuzwa kutokana na kile kinachotajwa kuwa ni
maofisa wa ardhi Jiji la Mbeya, kutumia fursa ya eneo hilo kujinufaisha
kwa kuuza viwanja.
Inaelezwa kuwa baadhi ya maofisa ardhi wa halmashauri ya jiji,
wamepima viwanja kwenye eneo hilo wakishirikiana na wakazi ambao ilikuwa
walipwe fidia kwa mashamba yao, na wakazi hao wanatumiwa kutafuta
wateja wa viwanja hivyo ili ionekane wao ndiyo walioviuza kwa watu
wanaojenga sasa.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla jana alitembelea eneo hilo
lililopo Veta jijini hapa na kujionea majengo yaliyojengwa kwenye ardhi,
iliyokuwa sehemu ya uwanja wa kujengwa Ikulu ndogo ya Mkoa.
Diwani wa Kata ya Ilomba, Dickson Mwakilasa alimwambia Mkuu wa Mkoa
kuwa eneo lilikojengwa nyumba za watu binafsi, lilikuwa na serikali na
kilichotakiwa ni kulipa fidia kwa wakazi waliokuwa na mashamba maeneo ya
jirani.
Kufuatia hali hiyo, Makalla alilazimika kuwahoji maofisa wa
halmashauri ya jiji, lakini wote wakaonekana kutoijua vyema historia ya
eneo hilo, hivyo ikamlazimu Mkuu huyo wa Mkoa kuahidi kufuatilia kwa
haraka nyaraka husika.
Alisema anachotaka kujua ni ramani inayoonesha ukubwa wa eneo la
awali; na pia matumizi yaliyopangwa, huku akisema anachojua yeye mpaka
sasa ni kuwa maofisa ardhi wameuza kinyemela sehemu ya uwanja wa Ikulu
ya Mkoa.
CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO
No comments:
Post a Comment