Social Icons

Wednesday, July 19, 2017

MAJALIWA AONYA MATAMSHI YA UCHOCHEZI


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Serikali itawashughulikia watu wote wanaotoa matamshi ya kichochezi nchini bila ya kujali nyadhifa zao. 
Amesema ni vema watu wakawa makini na kijiepusha kutoa matamshi ambayo yataathiri mfumo wa maisha kwa wananchi wengine.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo, Julai 19, wakati wa ibada ya mazishi ya mke wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, Linnah Mwakyembe iliyofanyika wilayani Kyela.
Amesema Serikali haitavumilia kuona baadhi ya watu wakitoa matamshi ambayo hayana tija kwa jamii na badala yake yanalenga kuwavuruga wananchi na kuchochea migogoro.
"Tutashughulika na watu wote wanaotoa matamshi ya kichochezi, popote walipo bila ya kujali uwezo wao, vyeo vyao na mamlaka walizonazo." 
Pia amewaomba viongozi wa dini waendelee kuliombea Taifa na viongozi wake na kwamba Serikali inawategemea na iko pamoja nao.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo baada ya Askofu wa Kanisa la Evangelical Brotherhood, Rabison Mwakanani kuonya vitendo vya baadhi ya watu kumtukana Rais John Magufuli.
Amesema ni vema watu hao wakajifunza namna ya kuwasilisha hoja zao bila ya kutumia lugha za matusi.
“Rais Magufuli amefanya mambo mengi makubwa kwa ajili ya maendeleo. Wanaofanya hivyo wasidhani kama wanamtukana Rais tu bali wanawatukana Watanzania wote waliomchagua wakiwemo viongozi wa dini,”amesema.
Pia aliwaomba wananchi kufanya maandalizi mapema kwa sababu wote ni wapitaji, hivyo waandae roho zao kwa kuacha kufanya dhambi na maovu yote ili wawe na mwisho mwema.
Waziri Mkuu pia amewaomba wananchi wote washirikiane kwa pamoja kumuombea . Mwakyembe na familia yake ili Mwenyezi Mungu aweze kuwafariji katika kipindi hiki kigumu.

Chanzo Mwananchi

No comments:

Post a Comment